MASOMO YA DOMINIKA YA 2 YA PASAKA: HURUMA YA MUNGU ISIYO NA KIKOMO!





“MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, April 28, 2019.
Dominika ya Pasaka (Dominika ya 2 ya Pasaka)

Acts 5: 12-16;
Ps 118: 2-4, 13-15;
Ufu: 1:9-19
Jn 20: 19-31.


HURUMA YA MUNGU ISIYO NA KIKOMO!


"Hakuna mtu atakayetengwa na huruma ya Mungu; kila mtu anajua njia ya kuipata huruma hiyo na Kanisa ni nyumba inayowakaribisha wote na hakuna anayekataliwa. Milango yake inabakia wazi, ili wote wanaoguswa na huruma waweze kupata toshelezo la msamaha. Dhambi inavyokuwa kubwa, vivyo hivyo upendo unapaswa Kuwa mkubwa ule ambao unatolewa na Kanisa kwa wale wote wanaoongoka... Kwa sababu hii, nimeamua kuitisha Jubilei ya hali ya pekee ambayo ni kuwa na huruma ya Mungu katika kiini chake. Unapaswa uwe mwaka mtakatifu wa Huruma. Twahitaji kuuishi mwaka huu katika mwanga wa maneno ya Bwana: "Kuwa na huruma, kama tu Baba yako alivyo na huruma. (Rej. Lk 6:36)." Haya yalikuwa ni maneno ya Papa Francis alipoutangaza mwaka 2016 kuwa ni "Mwaka Mtakatifu wa Huruma."

Leo katika Dominika ya Huruma ya Mungu, tunakumbushwa juu ya huruma ya Mungu isiyo na kikomo. Injili Leo inaonyesha mamlaka ya Yesu pale anapowapa mitume, Roho Mtakatifu, ambaye atakayetoa msamaha wa dhambi.

"Mungu hachoki kamwe kutusamehe; sisi ndiyo tunaochoka kuitafuta huruma yake. Yesu Kristo, aliyetuagiza tusameheane "saba mara sabini" (Mt 18:22) ametupa mfano wake yeye mwenyewe: ametusamehe saba mara sabini... kwa upole usiyotuacha tuaibike, lakini daima wenye uwezo wa kuturudishia furaha yetu, anatuwezesha kuinua vichwa vyetu na kuanza upya. Basi sisi tusiukimbie ufufuko wa Yesu, kamwe tusikate tamaa, hata litokee jambo gani. Maisha yake yawe mfano unaoangazia zaidi ya kitu chochote, unaotusukuma kwenda mbele!" (Furaha ya Injili, 3)

Sala: Bwana, Nisaidie kamwe nisiwe mbali nawe, badala yake niiamini huruma yako. Amina.



Copyright ©2013-2019 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com


IMANI





“MBEGU ZA UZIMA”
Jumapili, April 28, 2019.
Dominika ya Pasaka (Dominika ya 2 ya Pasaka)

Acts 5: 12-16;
Ps 118: 2-4, 13-15;
Ufu: 1:9-19
Jn 20: 19-31.


IMANI
Ndugu zangu imani ni muhimu sana katika maisha ya muumini kwa sababu maarifa yote tuliyonayo juu ya Mungu ni kwa njia ya imani.  Kwa imani tumekubali ujumbe wa mitume ambao waliishi na Bwana Yesu na walishuhudia mahubiri, uponyaji, msamaha, sala, mateso na kifo chake msalabani.
Katika Injili ya leo Bwana Yesu amewatokea mitume wake, ila Mtume Tomaso hakuwepo katika chumba ambacho milango yake ilifungwa kwa hofu ya Wayahudi baada ya vurugu zilizosababisha kusulubiwa na kufa kwake Bwana Yesu.  Nia ya Yesu Kristo ni kuwapa ujumbe wa amani na upatanisho.  Amani iwe kwenu… Pokeeni Roho Mtakatifu.  Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa, na wo wote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa, asema Bwana.  Huu ni mwito wa kuanza misheni mpya ya upatanisho.  Mara moja mitume wakaondoka wakamwambia Tomaso kwamba Tumemwona Bwana, akatusamehe kwa kumkana na kumwacha afe peke yake.  Tomaso alikataa kuamini akawaambia Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.  Ndipo Yesu akawatokea tena na kumwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako, uitazame mikono yangu, ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.  BWANA WANGU NA MUNGU WANGU, Tomaso alijibu.
Ndugu wapendwa tunajifunza katika Injili ya leo kwamba Mtume Tomaso aliamini kwa Yesu Mfufuka katika njia sawa na mitume wengine walivyoamini, anapomwona Bwana Yesu.  Zaidi ya hayo, Tomaso bado hakujazwa zawadi ya Roho Mtakatifu, hakuna mtu ambaye anaweza kumsadiki Bwana yesu bila msaada wa Roho Mtakatifu. Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu.  Tunaimarisha imani yetu tunaposali, tunapotafakari Neno la Mungu na tunapoishi maisha ya mwito wetu, yaani ikiwa tunaposhiriki katika maisha ya kikristo, kuhubiri ujumbe wa Bwana Yesu wa imani na upatanisho.
Je, katika maisha yetu ya kawaida tunaishije?  Je, tunayoamani mioyoni mwetu?  Je, tupo tayari kila wakati kuwasamehe wenzetu wanaotukosea kama vile Bwana Yesu alivyowasamehe mitume wake?  Baadhi yetu sisi wakristo hatuna amani katika maisha yetu.  Labda tunasumbuliwa mioyoni mwetu na baadhi ya mafundisho ya Kanisa ambayo yanatufanya tuwe na imani haba, kama vile Kutoa mimba, Uzazi wa mpango, Ugonjwa hatari wa Ukimwi, Kujizuia na tamaa za kimwili ili tujikinge na ukimwi.  Sisi wakristo tunafanya nini kuyaelewa zaidi mafundisho haya ya Kanisa?  Je, tunasoma kweli barua za Baba Mtakatifu juu ya hizi mada katika jumuiya zetu! Katika vikundi vyetu kama vile wakina mama, wakina baba, vijana, wanakwaya, Moyo Mtakatifu wa Yesu, Karismatik?  Ikiwa hatusomi barua hizo hatuwezi kujifunza mafundisho ya Kanisa Katoliki Takatifu.  Aidha hatuwezi kuwa na imani thabiti.
Maisha ya wakristo wa kwanza ni mfano bora kwetu sisi. Wakiwa chini ya uongozi wa mitume, wakristo hao waliishi maisha ya ushiriki, walikuwa wakipendana, wakisaidiana, wakisali na kushiriki Ekaristi Takatifu pamoja. Wakristo wa kwanza walikuwa na umoja, moyo mmoja na roho moja. Ndugu wapendwa leo tunaalikwa tuwe na imani thabiti kama wakristo wa kwanza.  Je, sisi tunashiriki namna gani katika jumuiya zetu? Je, kwenye jumuiya zetu tunapata faida gani?  Je, tunajifunza jinsi ya kusali na kutafakari Neno la Mungu katika jumuiya zetu?  Je, tunaadhimisha Ekaristi takatifu katika jumuiya zetu? Ikiwa hatufanyi haya yote kwenye jumuiya zetu hata katika familia zetu hatuwezi kukua kwa imani.  Ndiyo maana baadhi yetu hawashiriki pamoja nasi kwenye jumuiya  zetu.  Asilimia kubwa ya jumiya zetu sana sana ni mahali pa kujadiliana mambo ya fedha/pesa, zaka, michango, mizalisho, n.k. Baadhi ya jumuiya zetu ni mahali ambapo tunawaaibisha wenzetu kwa sababu hawatoi zaka, michango, kama hawajafika kufanya usafi Kanisani katika zamu yao. Hapana ndugu zangu, hatuwezi kujenga imani yetu katika vitu vya dunia bali tujenge imani yetu katika Yesu Mfufuka ambaye Mtume Tomaso hakusita kuamini alipohakikishiwa naye ukweli wa habari aliyosikia, akaungama BWANA WANGU NA MUNGU WANGU.
  Basi, tumwombe Yesu Mfufuka atusaidie kumwamini, kumpenda na kumuishi.


Copyright ©2013-2019 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

Comments

Popular posts from this blog

Mwanamume aliyekuwa amebeba cocaine kwenye makalio bandia ashikwa Ureno

Differences between Gymnosperms and Pteridophytes

Familia ya mwanafunzi Akwilina yataka haki itendeke